Wananchi wilayani Longido Mkoani Arusha wamelalamikia ongezeka kubwa la pikipiki za kubeba abiria lisilokwenda sambamba na mahitaji linalosababisha vijana wengi kuzitumia kusafirisha madawa ya kulevya,wahamiaji haramu na Majangili.
Wananchi hao wameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kudhibiti ongezekao la pikipiki hizo hasa maeneo ya mipakani ili kuepusha hali hiyo ambayo pia inachangia vijana wengi kufa kwa ajali wanapojaribu kuwakimbia askari na wengine kufungwa jela jambo linalowaongezea umaskini katika familia.
Baadhi ya wadau wanaosaidia vijana kukabiliana na umaskini katika maeneo ya vijijini wamesema ushirikiano zaidi wa kuwaepusha vijana kutumika kufanya uhalifu unahitajika ukiwemo wa kutoa elimu sambamba na kuwajengea mazingira ya kufanya kazi halali.
Akizungumzia hali hiyo kwa niaba ya mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Longido mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni mkuu wa kituo cha Polisi cha Longido Bw,John Hadu amesema kupitia ulinzi shirikishi wanaendelea kutoa mafunzo kwa waendesha pikipiki lakini tatizo bado ni kubwa likichangiwa pia na mazingira na pia uhaba wa watendaji.
Post a Comment